Antaktiki ni bara lililopo kwenye ncha ya kusini ya dunia, kati ya bahari za Pasifiki, Atlantiki na Bahari Hindi.
Jina "Antaktiki" linatokana na lugha ya Kigiriki likimaanisha "kinyume cha Aktiki", ambapo Aktiki ni eneo karibu na ncha ya kaskazini.
Bara hili lina eneo la kilomita za mraba milioni 14 na eneo hili limefunikwa karibu kabisa, yaani kwa asilimia 98% za eneo na theluji na barafu. Eneo lake ni kubwa kushinda Ulaya lakini hakuna mti hata mmoja. Bara hili linajulikana kama jangwa baridi.
Kwa sababu ya baridi kali katika bara hilo, ni bara pekee ambako binadamu hawaishi kwa namna ya kudumu, isipokuwa kuna watu 5,000, hasa wanasayansi, wanaokaa kwa muda katika vituo vyao.