Biotekinolojia ni aina ya tekinolojia inayotumia elimu ya biolojia kwa manufaa ya binadamu. Ni elimu pana sana inayoanza kwenye shughuli za kuchachusha mkate au pombe hadi kutumia mitambo ya hali ya juu katika maabara za kisasa.
Jina linatokana na maneno ya Kigiriki βιος (bios, uhai), τεγνɳ (technee, ufundi) na λογία (logia, elimu).
Tekinolojia hii hutumiwa hasa katika kilimo, uzalishaji wa vyakula na tiba. Viumbehai kama mimea na bakteria, dutu za kibiolojia kama vimeng'enya na kadhalika hutumiwa kwa kupata dutu, kemikali, mazao na bidhaa nyingine. Kuna pia maeneo mengine ambako biotekinolojia inafanyiwa majaribio.
Mara nyingi biotekinolojia hudhaniwa ilitokea juzijuzi tu kwa njia ya fani kama uhandisi jenetikia. Lakini hali halisi mbinu zake zimeshatumiwa tangu kale katika tamaduni zilizogundua njia za kufuga wanyama na kuzalisha mimea.