Eire Kaskazini ni eneo la kaskazini mashariki la kisiwa cha Ireland ambalo limo katika Ufalme wa Muungano, tofauti na sehemu kubwa ya kisiwa hicho iliyopata uhuru mwaka 1921.
Ni kwamba baada ya Vita vya uhuru vya Eire bunge la London kwa sheria ya mwaka 1920 (Government of Ireland Act 1920) liligawa Ireland katika sehemu mbili za Northern Ireland na Southern Ireland.
Wabunge waliochaguliwa katika Ireland ya Kusini walijitangaza kuwa bunge la Eire na kwa mapatano ya mwaka 1922 uhuru wa Eire ulitambuliwa. Nchi mpya ilijiita tangu 1937 "Jamhuri ya Eire" na kuendelea kama nchi ya pekee. Mikoa ya Northern Ireland iliendelea kuwa sehemu za Ufalme wa Muungano.
Ndani yake, mwaka 1999 Uskoti, Welisi na Ireland ya Kaskazini zilirudishiwa mabunge yao ya pekee.
Kadiri ya sensa ya mwaka 2021, wakazi ni 1,903,100[1] wanaoishi katika km2 14,130.
Wengi wao ni Wazungu (96.6%), wakifuatwa na Waafrika (0.6%), Wahindi (0.5%) na Wachina (0.5%).
Kiingereza ni lugha mama kwa asilimia 95.4 za wakazi.
Upande wa dini, wengi ni Wakristo (76.6%), hasa Wakatoliki (42.3%) na Waprotestanti wa madhehebu mbalimbali (37.3%). Wenye dini tofauti ni 1.3%, wakati 17.4% hawana dini yoyote au hawakujibu swali.