Hilali (kutoka Kiarabu هلال hilāl) ni neno la kutaja mwezi mpya au mwezi mchanga yaani mwezi jinsi unavyopatikana angani ukianza kuonekana tena baada ya hali ya kutoonekana inayotokea kila baada ya takriban siku 29. Hilali ina umbo la pinde nyembamba.
Jina hili linaangaliwa sana katika mazingira ya pwani ya Afrika ya Mashariki na pia kati ya wafuasi wa dini ya Uislamu maana katika kalenda ya Kiislamu kuonekana kwa hilali ni muhimu kwa hesabu ya mwezi mpya pamoja na sikukuu za dini hiyo. Kwa mfano, kufunga kwa mwezi wa Ramadhani kunaanza siku ambako hilali inaonekana baada ya mwezi wa nane Shaaban katika kalenda ya Kiislamu.