Istanbul (kwa Kituruki unatajwa İstanbul) ni mji mkubwa zaidi katika nchi ya Uturuki, ukiwa na wakazi wanaokadiriwa kuwa kati ya milioni 11 na 15, ambao wanaufanya kuwa miongoni mwa miji mikubwa ya dunia. Huu ndio mji mkuu wa Mkoa wa İstanbul.
Eneo la Istanbul linaelekea pande zote mbili za mlangobahari wa Bosporus unaotenganisha Ulaya na Asia. Hivyo ni mji pekee duniani uliopo katika mabara mawili.
Kiini cha kihistoria kipo upande wa Ulaya kwenye sehemu yenye umbo la rasi baina ya Bahari ya Marmara na Pembe ya Dhahabu ambayo ni mkono wa bahari unaoingia ndani ya nchi na hivyo mahali pa mji ulikingwa na bahari pande tatu.