Jeromu au Yeronimo (Strido, leo nchini Korasya 347 - Bethlehemu, Israeli, 420) alikuwa mmonaki, padri na mtaalamu wa Biblia, aliyemudu vizuri lugha zote za kitabu hicho pamoja na Kilatini hata akawa mwandishi bora wa lugha hiyo kati ya mababu.
Ujuzi wake huo mkubwa alioupata hasa Roma aliposoma na kubatizwa, ulimwezesha kutafsiri na kufafanua Biblia vizuri sana.
Kisha kupatwa na mvuto mkubwa kwa maisha ya sala, alishika juhudi, akahamia Mashariki ya Kati, akapadirishwa.
Aliporudi Roma, akawa katibu wa Papa Damaso I, halafu akahamia moja kwa moja Bethlehemu wa Yuda kuishi kimonaki. Hata hivyo aliendelea kujihusisha na mahitaji mbalimbali ya Kanisa hadi kifo chake uzeeni[1].
Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.
Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.
Sikukuu yake inaadhimishwa tarehe 30 Septemba[2].