Kaaba ni jengo lenye umbo la mchemraba lililopo ndani ya msikiti mkuu wa Masjid al-Haram mjini Makka nchini Saudia.
Inatazamwa kama mahali patakatifu katika imani ya Uislamu. Waislamu huamini ni nyumba ya Mungu iliyojengwa kiasili na Adamu na baadaye na Abrahamu.
Ni lengo la safari ya hija. Kila Mwislamu mwenye uwezo anatakiwa kuitembelea angalau mara moja katika maisha yake.
Waislamu wanatakiwa kuielekea Kaaba wakati wa kusali na kila msikiti huwa na sehemu ya mihrabu inayotazama Makka. Mwelekeo huu huitwa kibla.