Kisomali (kwa mwandiko wa Kilatini: Af-Soomaali; Osmanya: 𐒖𐒍 𐒈𐒝𐒑𐒛𐒐𐒘 [æ̀f sɔ̀ːmɑ́ːlì]) ni lugha ya Kiafrika-Kiasia nchini Somalia, Ethiopia, Kenya na Jibuti inayozungumzwa na Wasomali.
Kupitia kwa Wasomali wahamiaji, Kisomali huzungumzwa katika nchi nyingine nyingi kama vile Kanada, nchi mbalimbali za Ulaya na za Uarabuni.
Mwaka wa 2006 idadi ya wasemaji wa Kisomali nchini Somalia ilihesabiwa kuwa watu 8,340,000. Pia kuna wasemaji 4,610,000 nchini Ethiopia (2007), 2,386,222 nchini Kenya (2009), na 297,200 nchini Jibuti (2006).
Kufuatana na uainishaji wa lugha kwa ndani zaidi, Kisomali kiko katika kundi la lugha za Kikushi.
Lugha ya Kisomali imeandikwa rasmi kwa alfabeti ya Kilatini ingawa alfabeti ya Kiarabu na maandishi kadhaa ya Kisomali kama vile Osmanya, Kaddare na maandishi ya Borama yanatumiwa kwa njia isiyo rasmi.