Kwa maana nyingine ya neno hili angalia hapa Kitanda (maana)
Kitanda ni samani ya kulala au kujipumzisha inayopatikana kwa kawaida katika kila nyumba.
Asili ya neno "kitanda" ni mzizi "-tanda".
Katika utamaduni wa Waswahili kitanda ni samani kubwa. Ina kiunzi au fremu ya ubao, yenye vitakizo viwili upande wa kichwa na mguuni vinavyoshikwa kwa mifumbati kila upande. Yote inakaa juu ya matendegu (miguu ya ubao) manne. Nafasi kati ya mifumbati inafumaniwa kwa kamba, usumba wa nazi au nyasi. Juu ya hii huwekwa mkeka au godoro. Vitakizo mara nyingi hupambwa kwa vioo vya rangi au vyenye picha. Kiunzi cha juu kinaweza kufunikwa kwa vitambaa au chandarua.
Ukubwa wa kitanda hutofautiana. Kuna kitanda kidogo cha mtoto, vitanda vya kawaida vya kulaliwa na mtu mmoja na pia kitanda kikubwa zaidi cha kulaliwa na watu wawili[1].