Kuku | ||||||||||||||||||
---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|---|
Kuku: Jogoo na tembe
| ||||||||||||||||||
Uainishaji wa kisayansi | ||||||||||||||||||
|
Kuku (Gallus gallus domesticus) ni ndege anayefugwa na binadamu nyumbani tangu miaka 8,000 hivi. Kwa sababu hiyo ni miongoni mwa wanyama waliosambaa zaidi duniani na ndio ndege walio wengi zaidi duniani.[1]
Watu hutumia nyama yake na mayai kama chakula. Mwanzoni kuku walifungwa kwa ajili ya mchezo wa mapigano ya kuku na kwenye sherehe maalumu. [2]Katika nchi za baridi malaika yao, ambayo ni manyoya madogo ya chini, yanatumiwa kwa kujaza mashuka au makoti. Samadi ya kuku ni mbolea nzuri lakini inapaswa kukaa kwa muda kabla ya kutumiwa.
Idadi ya kuku duniani inakadiriwa kuwa zaidi ya bilioni 10 (mpaka kufikia bilioni 24 mwaka 2003) na wengi wanafugwa kwa wingi wakiotamiwa na kuishi zizini. Kwa njia ya ufugaji aina nyingi za kuku zimeendelezwa kwa kuchagua wale wenye tabia maalumu na kuzaliana. Wanaofugwa siku hizi ni aina zinazotoa hasa nyama na aina nyingine zinatoa hasa mayai.
Kuku dume huitwa jogoo na jike ni tembe; mtoto wa kuku ni kifaranga. Kutokana na ufugaji uwezo wa kuruka umepotea.
Katika mazingira asilia kuku huishi miaka 5-11 lakini wale wanaofugwa kwa wingi wanachinjwa baada ya wiki 6-8 kama ni kuku wa nyama na baada ya mwaka mmoja kama ni kuku wa mayai. Kati ya aina zinazofugwa kwa mayai karibu madume wote, yaani nusu ya vifaranga, wanauawa mara moja kwa sababu hawatagi mayai na aina hii haileti nyama ya kutosha.
Asili ya kuku zetu ni kuku-mwitu mwekundu wa Asia ya Kusini-Mashariki. Ilisemekana kuwa, kuku walianza huko India, lakini ushahidi wa sasa unaonyesha kuwa walianza huko Vietnam miaka 10,000 iliyopita. Ufugaji wake ulisambazwa Asia Bara na Polynesia. Mabaki ya mifupa ya kuku yamepatikana China yakiwa na umri wa miaka 8,000. Kutoka Asia ya Kusini-Magharibi kuku walisambazwa pia Uhindi na kupitia Uajemi hadi Ugiriki na sehemu nyingine za Ulaya, Misri n.k. Inaaminiwa ya kwamba kuku waliletwa Amerika Kusini kabla ya kuja kwa Kolumbus kupitia Pasifiki.