Kupanda kwa halijoto duniani (ing. global warming) ni mchakato wa mabadiliko ya tabianchi yaliyotambuliwa na wataalamu tangu miaka kadhaa.
Mchakato huo ulianza pamoja na usambazaji wa viwanda duniani. Unaonekana kwa kulinganisha vipimo vya halijoto vinavyopatikana tangu miaka 150. Kupanda huku kunaleta mabadiliko ya hali ya hewa yaliyoanza tayari kuathiri maisha ya watu na uhai kwa ujumla.
Kuna hofu ya kwamba mabadiliko hayo yataleta hatari kubwa kwa jamii.
Kati ya wanasayansi kulikuwa na majadiliano kama sababu za mabadiliko hayo ni shughuli za binadamu tu au kama kuna sababu asilia. Siku hizi wataalamu karibu wote hukubaliana ya kwamba sababu kuu ni kuchoma kwa makaa na mafuta katika viwanda, magari na vituo vya umeme kunakopuliza hewani gesijoto kama dioksidi kabonia.