Maji ni kimiminika ambacho ni kiini cha uhai wowote duniani na pia kiini cha utamaduni wa binadamu. Hakuna mtu anayeweza kuishi bila maji kwa sababu asilimia 50 - 65 za mwili wa mwanadamu ni maji. Hata miili ya mimea na wanyama kwa kiasi kikubwa ni maji. Pia katika dunia maji yamechukua karibu robo tatu ya eneo lake lote (71.11%). Kwa hiyo maji ni kitu cha msingi sana.
Kiasi kikubwa cha maji duniani ni maji ya chumvi katika bahari; maji matamu yanayoweza kutumiwa na binadamu na kwa kilimo ni asilimia ndogo tu ya maji kwenye Dunia.
Maji yana matumizi mengi nyumbani na katika uchumi: nyumbani maji hutumika katika kunywa, kuogea, kuoshea vitu na vyombo mbalimbali; kiuchumi maji yanatumika viwandani, kwa mfano kupoozea au kuoshea mashine, pia maji hutumika katika usafiri, kama vile meli za mizigo, za abiria na vinginevyo.
Katika matumizi hayo pengine watu hutumia vibaya maji na vyanzo vyake ambavyo ni muhimu vitunzwe kwa kuwa tukiharibu vyanzo hivyo twaweza kuleta hali ya jangwa katika eneo hilo.