Monasteri (kutoka Kiingereza "monastery") katika Ukristo ni jengo au majengo ya pamoja ambapo inaishi jumuia ya wamonaki, chini ya mamlaka ya abati. Kila moja inaweza kujitegemea, ingawa pengine yameundwa mashirikisho ili kusaidiana na kuratibu malezi na masuala mengine ya pamoja.
Monasteri ni tofauti na konventi, zilizoanzishwa na mashirika ya ombaomba, ambayo wanajumuia wake si wamonaki bali wanaitwa "ndugu".
Monasteri za Kikristo zilianza kujengwa baada ya kwisha kwa dhuluma za Dola la Roma dhidi ya Ukristo, ingawa hata kabla ya hapo kulikuwa na waamini wanaoishi namna fulani ya maisha ya kitawa.
Kwa karne nyingi monasteri zilikuwa kama mji mdogo unaojitegemea kiuchumi pia kutokana na mkazo uliowekwa katika kusali na kufanya kazi.
Kuna monasteri hata katika ya baadhi ya dini nyingine, hasa Ubuddha.