Chanzo | Ziwa Ontario, 44°06′N 76°24′W / 44.100°N 76.400°W |
Mdomo | Ghuba ya Saint Lawrence, Atlantiki |
Nchi | Kanada, Marekani |
Urefu | km 500 |
Mkondo | 16,800 m3/s |
Miji mikubwa kando lake | Montreal, Quebec |
Mto Saint Lawrence (kwa Kiingereza: Saint Lawrence River, kwa Kifaransa: Fleuve Saint-Laurent) ni mto mkubwa katika Amerika ya Kaskazini. Mwanzoni unafuata mpaka baina ya Kanada na Marekani halafu unapita katika jimbo la Quebec hadi kuishia katika Ghuba ya Saint Lawrence na Bahari Atlantiki.
Chanzo chake kipo pale unapoondoka katika Ziwa Ontario. Lakini ilhali maziwa makubwa ya Amerika Kaskazini yote yameunganika, maji ya maziwa hayo yote huelekea baharini kupitia mto Saint Lawrence. Kwa hiyo inawezekana kuhesabu vyanzo vyote vya maziwa hayo kuwa vyanzo vya mto Saint Lawrence, na kwa mtazamo huu urefu wake ni zaidi ya kilomita 3,000.
Mdomo wake ni mpana sana na huitwa Ghuba ya Saint Lawrence. Umbali baina ya Ziwa Ontario na Ghuba ya Saint Lawrence ni kilomita 500.
Upande wa Kanada kuna miji ya Kingston, Montreal, Trois-Rivières na Quebec City kando ya mto huu. Meli kubwa zinaweza kuutumia kama njia baina ya Maziwa Makuu na Atlantiki.