Munyu au chumvi ya kawaida (wakati mwingine pia chumvi ya mezani; kwa Kiing. table salt) ni madini yanayotumik kama kiungo cha chakula.
Munyu ni mojawapo ya chumvi za kikemia. Ni hasa kampaundi ya kloridi ya natiri (sodium chloride) inayofanywa na atomu moja ya klorini na atomu moja ya natiri na huwakilishwa na alama NaCl.[1] Ikitokea kwenye maji ya bahari au kwenye migodi viwango vidogo vya madini mengine vinaweza kuwemo. Katika nchi nyingi kiasi kidogo cha iodini huongezwa kwenye munyu ili kuzuia ugonjwa wa kororo.[2].
Umbo lake la kawaida ni fuwele. Inapatikana chini ya ardhi kama matabaka ya miamba inapochimbwa katika migodi. Kwa matumizi ya binadamu hutolewa pia kwenye maji ya bahari ambamo ni takriban asilimia 3-4 ya masi yake[3]. Mahali pengi hupatikana pia kwa umbo la maji ya chumvi lenye sehemu ambako chemchemi hutokea penye miamba ya chumvi chini ya ardhi, kama vile huko Uvinza kwenye Mkoa wa Kigoma. Maji ya chumvi huchemshwa au huachwa katika beseni kubwa ambako yanakauka na chumvi inabaki.
Inatumiwa sana na binadamu kwa sababu mwili unahitaji kuongeza madini ndani yake. Hivyo watu husikia inaboresha ladha ya vyakula. Lakini kuongezeka kwa munyu mwilini kunaleta pia hatari za afya.[4]
Chumvi hii huwa na matumizi mengine mengi katika maisha ya kila siku, kwa mfano katika kuhifadhi vyakula mbalimbali, ngozi n.k.