Mwezi mwandamo (kwa Kiing. New Moon) ni awamu ya Mwezi ambapo hauonekani kwa macho. Awamu hiyo inatokea kila baada ya siku 29 1/2.
Katika awamu hiyo Mwezi uko kati ya Dunia na Jua. Hivyo ni nusu ya Mwezi isiyoonekana kutoka Duniani ndiyo inayopokea nuru ya Jua lakini upande ambao tunatazama uko kivulini[1].
Hali halisi upande unaotazama Dunia hauko gizani kabisa kwa sababu unapokea kiasi cha nuru inayoakisiwa kutoka uso wa Dunia. Lakini wakati wa mchana nuru ya Jua ni kali zaidi hivyo hatuoni Mwezi.
Ilhali Mwezi uko kati ya Jua na Dunia, kuna hali ya pekee. Kama Mwezi unapita kamili mstari uliopo baina ya Jua na Dunia, unafunika Jua kwa muda mfupi. Kwa njia hiyo kivuli cha Mwezi kinapita kwenye uso wa Dunia. Watu waliopo katika eneo la kivuli chake wanaona kupatwa kwa Jua[2].