Neno nabii (kwa Kiebrania נביא nevì, kwa wingi נְבִיאִים nevi'ìm, kwa Kiarabu نبي) linatumika kumtajia binadamu anayesema kwa niaba ya Mungu, hasa kwa kusudi la kuelekeza wenzake wafuate imani na maadili sahihi.
Katika lugha nyingi, mtu huyo anaitwa kwa jina linalotokana na neno la Kigiriki προφήτης [prophētēs], maana yake "anayesema mbele", yaani hadharani (mbele ya wasikilizaji), au kabla ya (jambo kutokea).
Watu wa namna hiyo wanapatikana katika dini nyingi, hususan katika Uyahudi, Ukristo na Uislamu.
Katika matumizi ya kawaida, neno hilo linatumika hasa kwa mtu ambaye anatabiri jambo, bila ya kujali asili ya maarifa yake.