Ngome ya Yesu (pia: Boma la Yesu; kwa Kiingereza: Fort Jesus) ni ngome ya kale mjini Mombasa (Kenya). Iko kwenye kisiwa cha Mombasa ikitazama mlango wa bandari ya kale.
Ilijengwa mwaka 1593 na msanifu Giovanni Battista Cairato kwa niaba ya Wareno na ilikuwa kituo muhimu cha Wareno kwenye njia ya mawasiliano kati ya Ureno na Uhindi. Jahazi zao zilipita Afrika Kusini zikapumzika kidogo Msumbiji penye ngome kubwa ya Kireno halafu ziliendelea kupitia Mombasa na kuvuka bahari hadi Bara Hindi.