Mapezi ni sifa bainifu sana za mwili wa samaki. Hushirikishwa kwa miiba au tindi za mfupa zinazotokeza katika mwili na kufunikwa na kuunganishwa pamoja na ngozi, ama katika mtindo wa utando, kama inavyoonekana katika samaki wengi wenye mifupa, au sawa na kikono, kama inavyoonekana katika papa. Licha ya mkia au pezimkia, mapezi ya samaki hayana muungano wa moja kwa moja na uti wa mgongo na hutegemewa tu na misuli. Kazi yao kuu ni kusaidia samaki kuogelea. Mapezi yaliyomo katika sehemu tofauti kwenye samaki hutumikia madhumuni tofauti kama kusonga mbele, kugeuka, kukaa wima au kusimama. Takriban samaki wote hutumia mapezi wakati wa kuogelea, panzi-bahari hutumia mapeziubavu kwa kuumbia, na guguye huyatumia kwa kutembea. Mapezi pia yanaweza kutumika kwa madhumuni mengine; papa na msiha-mbu hutumia pezi lililobadilika ili kufikisha shahawa, karage hutumia pezimkia lao ili kuziraisha mawindo, mabocho wana miiba katika mapezimgongo yao yanayoingiza sumu, samaki washawishi hutumia mwiba wa kwanza wa pezimgongo lao kama fimbo ya uvuvi ili kuvutia mawindo, na vikande huepuka mbuai kwa kujifinya ndani ya ufa za miamba ya korali na kutumia miiba katika mapezi yao ili kujifunga kwenye mahali palepale.