Upepo wa Jua (kwa Kiingereza solar wind) ni jina la mkondo mfululizo wa chembe za nyuklia unaotoka katika Jua. Chembe za nyuklia ni vipande vidogo vinavyopatikana ndani ya atomi. Upepo wa Jua ni hasa mkondo wa protoni, elektroni na viini vya heliamu wenye kasi inayotosha kutoka nje ya graviti ya Jua. Mchanganyiko huo wa chembe huitwa plasma (utegili): ni kama gesi inayoundwa na ioni. Hii ndiyo sababu ya kwamba upepo wa Jua ni mkusanyiko wa chembe zenye chaji ya umeme.
Mkondo wa chembe kutoka Jua, yaani upepo wa Jua, hutokea muda wote lakini nguvu yake inabadilika. Kwa wastani kwa njia hiyo kila sekunde Jua linapotewa na tani 1,000,000 za mata yake kuingia kwenye anga-nje. Wakati wa milipuko kwenye uso wa Jua (inayotokea mara kwa mara) idadi hiyo inaongezeka sana na hapo upepo wa jua unaweza kuitwa dhoruba ya jua.
Upepo wa Jua unatokea pia nje ya mfumo wa Jua letu kwa majua au nyota nyingine. Hapo unaitwa "upepo wa nyota" (ing. stellar wind) lakini kimsingi ni jambo lilelile, ila tu mbali sana.