Yoshua (kwa Kiebrania: יְהוֹשֻׁעַ, Yəhōšuaʿ au Yŏhōšuaʿ, yaani 'YHWH ni wokovu'[1][2], lakini pia יֵשׁוּעַ, Yēšūaʿ; kwa Kiaramu: ܝܫܘܥ ܒܪ ܢܘܢ, Yəšūʿ bar Nōn; kwa Kigiriki: Ἰησοῦς, Yesus; kwa Kiarabu: يُوشَعُ ٱبْنُ نُونٍ, Yūšaʿ ibn Nūn; kwa Kilatini: Iosue au Josue[3]), mwana wa Nun, mtumishi wa Mungu, alikuwa kiongozi wa taifa la Israeli baada ya Musa aliyemwekea mikono kichwani ili ajazwe roho ya hekima. Hivyo, kupitia mto Yordani, aliweza kuingiza Waisraeli katika nchi ya Kanaani na kuiteka kwa namna ya ajabu[4].
Anajulikana hasa kupitia kitabu cha sita kati ya vitabu vya Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na vya Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.
Kitabu hicho chenye sura 24 kinatupasha habari za uvamizi wa nchi takatifu ambao Waisraeli waliufanya chini ya Yoshua, ambaye ni mfano wa Yesu (hata jina lao kwa Kiyahudi ni moja, linalotafsiriwa “Mungu anaokoa”): kwa imani ya Wakristo, Yesu ndiye aliyewaingiza watu katika nchi ya ahadi, si Musa.
Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.
Yoshua anaheshimiwa kama mtakatifu na Wayahudi, Wakristo na Waislamu, hasa tarehe 1 Septemba[5].