Daladala ni neno la kawaida nchini Tanzania la kutaja gari dogo linalotumika kwa usafiri wa umma likifuata njia maalumu yenye namba yake.
Dereva anafanya kazi yake pamoja na msaidizi anayeitwa "konda" au "manamba"[1] mwenye kazi ya kukusanya pesa na kufungua au kufunga mlango.
Nchini Kenya magari hayo yanaitwa matatu.
Kwa muda mrefu sasa daladala zimekuwa ni mkombozi wa watu wengi katika kurahisisha shughuli nzima ya usafirishaji. Mwanzoni mabasi yaliyotumika zaidi yalikuwa ni Hiace ambapo Watanzania wakatohoa na kuyaita mabasi hayo "Vihaisi" au "Vipanya".[2] Muda ulivyozidi kwenda hali ikabadilika kwani miji ilikua na kutanuka na watu kuongezeka, hivyo usafiri huo ukawa wa kwenda barabara za ndani huku barabara kubwa zikitawaliwa na mabasi makubwa, haswa mabasi aina ya Costa na Toyota DCM au Dyna Clipper.[3]