Kivusho au Kivuko (kutoka kitenzi "kuvuka") au Pantoni (kutoka Kiingereza "pontoon") ni boti au meli inayobeba watu na mizigo kuvuka ziwa, mito na sehemu za bahari.
Istilahi hizi zinatumiwa pamoja; pale Dar es Salaam ni kawaida kusema "pantoni" ya kuvukia Kigamboni (yaani kupitia mdomo wa bandari) na "feri" kwenda Zanzibar hata kama pantoni moja ya Kigamboni ni kubwa kuliko boti kadhaa zinazoelekea Unguja,
Kuna feri ndogo zinazohudumia watu wanaoishi mtoni pasipo daraja. Huko kuna uwezekano wa kuendesha feri bila injini kwa kutumia mwendo wa mto wenyewe. Feri hizo zinahitaji kamba au waya kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Feri kubwa zaidi hubeba pia magari na malori pamoja na abiria. Pasipo madaraja kuna feri za pekee za kubeba treni.
Visiwa maziwani au baharini mara nyingi vinategemea feri kwa mawasiliano na bara.
Feri zinapatikana pia kwenye milango ya bahari au kwenye midomo ya hori.
Katika miji inayotumia njia za maji kama Venisi feri ndogo zinafanya kazi kama daladala, matatu au mabasi ya mjini.
Vyombo hivi vilisaidia sana na bado vinasaidia kuvusha watu katika vyanzo mbalimbali vya maji.
Siku hizi pantoni hazitumiki sana kwa sababu ya teknolojia mpya ya ujenzi wa madaraja makubwa yanayoweza kukatiza katikati ya vyanzo vikubwa vya maji, kwa mfano maziwa, mito, bahari.
Pantoni bado zinatumika sana katika nchi za Afrika kwani teknolojia hii bado haijasambaa, nchi kama vile Tanzania bado pantoni zinatumika kuvusha watu kutoka ng'ambo moja kwenda ng'ambo nyingine.
Pantoni inabeba watu na vitu kulingana na ukubwa wake; kwa mfano kivuko cha MV Magogoni cha Dar es Salaam kinaweza kubeba watu elfu moja na zaidi pamoja na magari madogo 30-40.