Kanisa la Moravian (kwa Kiingereza: Moravian Church; pia: Umoja wa Ndugu kutoka jina la kihistoria la Kilatini "Unitas Fratrum", au ndugu wa Herrnhut) ni madhehebu ya Ukristo wa Kiprotestanti yaliyoanzishwa mwaka 1722 katika Ujerumani na wakimbizi kutoka Moravia.
Baadaye yakaenea katika nchi nyingi kwa juhudi kubwa za kimisionari; leo hii ni kanisa dogo kimataifa, lakini nchini Tanzania ni la tatu kwa ukubwa kati ya makanisa ya Kiprotestanti baada ya Walutheri na Waanglikana. Idadi kubwa ya Wakristo Wamoravian huishi Tanzania.
Katika mafundisho yake hukazia umoja wa Wakristo na ushirikiano kati ya madhehebu mbalimbali, imani ya Mkristo binafsi, uenezaji wa imani ya kikristo na muziki.
Umoja wa Ndugu ni muungano wa majimbo ya kujitegemea yanayoshirikiana chini ya katiba ya kanisa. Uongozi ni mikononi mwa sinodi ya umoja inayokutana kila baada ya miaka 7. Kamati ya umoja ina mjumbe mmoja kutoka kila jimbo.
Nembo lake ni alama ya mwanakondoo wa Mungu anayeshika bendera ya ushindi pamoja na maandishi ya Kilatini: Vicit agnus noster, eum sequamur inayotafsiriwa kama "Mwanakondoo wetu ameshinda, tumfuate" (kwa Kiingereza: "Our Lamb has conquered, let us follow Him").