Kilimanjaro ni jina la mlima mrefu kuliko yote barani Afrika. Mlima huo uko nchini Tanzania katika Mkoa wa Kilimanjaro. Una urefu wa mita 5,895 (futi 19,340).
Hali halisi Kilimanjaro ni zaidi ya mlima tu, ni kama safu ndogo ya milima mitatu: Kibo, Mawenzi na Shira. Hiyo mitatu inaonekana kama vilele vitatu vya mlima mmoja, hivyo si vibaya kusema Kilimanjaro ni mlima.
Kijiolojia Kilimanjaro ni volkeno iliyolala kwa sasa. Kwenye kilele cha Kibo gesi bado inatoka. Kumbukumbu ya wenyeji ina habari ya mlipuko mnamo mwaka 1730.
Kilele cha juu cha Kibo kinaitwa Uhuru. Mtu wa kwanza kufika kileleni hapo alikuwa Johannes Kinyala Lauwo kutoka Marangu aliyewaongoza Wajerumani Hans Meyer na Ludwig Purtscheller tarehe 6 Oktoba 1889 wakati wa ukoloni wa Ujerumani. Wakati ule waliita ncha ya juu "Kaiser-Wilhelm-Spitze" (kwa Kijerumani: Kilele cha Kaisari Wilhelm) kwa heshima ya Kaisari wa Ujerumani.