Liturujia ya Ugiriki, iliyoenea kutoka Konstantinopoli, sasa Istanbul (nchini Uturuki) ni liturujia ambayo lugha yake asili ni Kigiriki, lakini siku hizi inaadhimishwa katika lugha nyingine nyingi kukiwa na tofauti ndogondogo duniani kote.
Wanaoitumia hasa ni Waorthodoksi wote na baadhi ya Makanisa Katoliki ya Mashariki: hivyo ni ya pili kwa uenezi baada ya liturujia ya Roma.
Vitabu vyake vinaongoza Liturujia ya Kimungu (Ekaristi), Vipindi vya sala rasmi, Mafumbo matakatifu (Sakramenti) na sala, baraka na mazinguo mbalimbali, vilivyostawi katika Kanisa la Konstantinopoli.
Liturujia hiyo inahusika pia na namna maalumu za usanifu majengo, picha takatifu, muziki wa liturujia, mavazi na mapokeo zilizostawi vilevile karne hata karne kila ilikotumika.
Kwa kawaida mkusanyiko wa waamini huwa wamesimama muda wote wa ibada, na ukuta wa picha takatifu unaoitwa iconostasis unawatenganisha na patakatifu anapohudumia askofu au padri akisaidiwa na shemasi.
Ushiriki wa walei unajitokeza katika kusujudu mara nyingi na kuitikia sala na nyimbo.
Katika liturujia hiyo Biblia inatumika sana katika masomo na katika matini mengine vilevile.
Taratibu za saumu ni kali kuliko zile za Ukristo wa Magharibi na zinafuatwa katika vipindi vinne kwa mwaka: Kwaresima Kuu, Kwaresima ya Noeli, Mfungo wa Mitume na Mfungo wa Kulala kwa Bikira Maria. Pamoja na hayo, Jumatano na Ijumaa nyingi ni za kufunga chakula. Monasteri nyingi zina mfungo hata Jumatatu zote.