Mapambano ya uhuru Tanganyika ni yale yaliyofanyika katika Tanzania bara ya leo dhidi ya ukoloni.
Tanganyika, kama nchi yenye mipaka maalumu, ilianzishwa baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, ilipokuwa chini ya mamlaka ya Uingereza.
Kabla ya hapo ilikuwa sehemu ya koloni la Afrika ya Mashariki ya Kijerumani, pamoja na nchi za leo Rwanda na Burundi.
Baada ya kuvamiwa na majeshi ya wapinzani wa Ujerumani wakati wa vita, Shirikisho la Mataifa lilikabidhi sehemu kubwa ya makoloni ya Kijerumani kwa Uingereza na nchi nyingine kama "eneo la kudhaminiwa". Serikali ya Uingereza iliamua kutumia jina "Tanganyika" kufuatana na jina la ziwa kubwa kwenye mashariki ya eneo.