Martyrologium Romanum (kwa Kilatini: Kitabu cha Wafiadini cha Roma) ni kitabu rasmi cha liturujia ya Roma kwa kufanya siku kwa siku ukumbusho wa watakatifu wanaoheshimiwa na Kanisa Katoliki. Ni msingi wa kalenda ya watakatifu katika mwaka wa liturujia.
Kinatunza orodha rasmi lakini isiyodai kuwa kamili, hivi kwamba majimbo, nchi na mashirika vinaweza kuwa na nyongeza maalumu za kwao.
Toka zamani jina Martyrologium lilitumika kwa orodha za watakatifu na wenye heri waliopangwa kadiri ya tarehe ya sikukuu zao. Polepole vitabu vya mahali tofauti viliongezewa majina kutoka vitabu vingine na hatimaye mikusanyo ilifikia kiwango cha kimataifa.
Katika Kanisa la Kiorthodoksi, kitabu cha namna hiyo kinaitwa Synaxarion, na toleo refu zaidi Menologion.
Toleo rasmi la Kanisa la Roma liliidhinishwa mara ya kwanza na Papa Gregori XIII mwaka 1584. Limetolewa upya mwaka 2001 halafu 2004[1] kwa kuzingatia zaidi ushahidi wa historia kama ulivyoagiza Mtaguso wa pili wa Vatikano [2]. Toleo hilo linaorodhesha watu 7,000 hivi.