Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula (pia: mwanya wa chakula[1]) ni jumla ya viungo mwilini mwa binadamu na mamalia wengine vinavyofanya kazi ya kuingiza chakula mwilini, kukisagasaga, kukisafirisha ndani ya mwili, kukimeng'enya, kuondoa lishe ya mwili ndani yake, na kutoa mabaki nje ya mwili. Kwa hiyo mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni njia yote kuanzia mdomo hadi mkundu.
Magonjwa yake huchunguzwa na elimu ya gastro-enterolojia.
Kwa lugha nyingine unahusika na umeng'enyaji wa chakula mpaka kuwa katika hali inayoweza kusharabiwa na mwili. Ili chakula kiweze kutumika mwilini, ni lazima kivunjwevunjwe kiwe katika hali rahisi ya kuweza kusharabiwa. Kazi hiyo hufanywa na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mwanadamu hufanana na ule wa sungura, panya au pimbi. Sehemu kuu zinazohusika katika umeng’enyaji huo ni kinywa, umio, mfuko wa tumbo, ini, mfuko wa nyongo, utumbo mwembamba, kongosho, utumbo mpana na puru.
Chakula kinaposafiri katika njia yake hufanyiwa mabadiliko ya kiumbo na ya kikemikali. Kila sehemu ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ina kazi maalum. Chakula cha mnyama au binadamu huweza kuwa cha kabohaidreti/wanga, protini, mafuta au mchanganyiko wa viambato hivyo. Myeyuko wa makundi hayo ya vyakula hutokea katika sehemu mbalimbali za njia ya chakula kwa njia za kemikali.