NSDAP ni kifupi cha Nationalsozialistische Deutsche Arbeiterpartei (Chama cha Kizalendo - Kisoshalisti cha Wafanyakazi Wajerumani) kilichotawala Ujerumani kuanzia 30 Januari 1933 hadi 8 Mei 1945 wakati wa udikteta wa kiongozi wake Adolf Hitler. Chama chenyewe kilitumia pia kifupi cha "NS" kwa harakati yake na vitengo vyake.
Chama hiki kinachojulikana pia kama Chama cha Nazi (tamka: natsi) kilianzishwa mjini München (Munich) 1919 kwa jina la Deutsche Arbeiterpartei (Chama cha Wafanyakazi Wajerumani) (DAP). Jina likabadilishwa 1920 kuwa NSDAP. Sababu za kuanzishwa kwa chama zilikuwa mipango ya matajiri wenye mwelekeo wa kizalendo waliotaka kujenga harakati dhidi ya vyama vya kijamaa vyenye wafuasi wengi kati ya wafanyakazi. Walitegemea ya kwamba chama kinachoitwa cha wafanyakazi na cha kizalendo kitapunguza athira ya Wajamaa na Wakomunisti kati ya wafanyakazi.
Hadi mwaka 1923 chama kilikua katika jimbo la Bavaria lakini hakikuwa na athira kubwa nje ha hapa.