Novaya Zemlya (kwa Kirusi Но́вая Земля́, yaani Nchi mpya) ni funguvisiwa la Urusi lililopo kwenye Bahari Aktiki. Eneo lake ni kilomita za mraba 90,650. Kiutawala ni Wilaya ya Novaya Zemlya katika mkoa wa Arkhangelsk Oblast. [1].
Mwaka 2010 ilikuwa na wakazi 2,429 na kati yao karibu 2,000 waliishi katika mji wa Belushya Guba, makao makuu ya wilaya.
Wakazi asilia walikuwa wawindaji na wavuvi wa kabila la Wanenets waliohamishwa kutoka visiwa katika miaka ya 1950 [2]. Wakati ule walikuwa watu wasiozidi 300. [3]. Uhamisho huo ulisababishwa na mipango ya kutumia visiwa kwa shughuli za kijeshi na majaribio ya kulipua mabomu ya nyuklia.
Novaya Zemlya kuna visiwa viwili vikubwa vinavyotenganishwa na mlangobahari mwembamba wenye upana wa mita 600 hadi kilomita chache.
Mlima mkubwa uko kwenye kisiwa cha kaskazini wenye kimo cha mita 1,547.
Hadi leo Novaya Zemlya ni kituo cha kijeshi na wakazi wengi ni wanajeshi pamoja na familia zao. Umoja wa Kisovyeti ulitumia visiwa kwa milipuko ya majaribio ya mabomu ya nyuklia; tarehe 30 Oktoba 1961 mlipuko mkubwa wa kinyuklia katika historia ulitekelezwa hapa. Nguvu ya bomu ilikadiriwa kuwa na megatoni 50.