Nuru (kutoka Kiarabu نور, nur; pia mwanga) ni neno la kutaja mnururisho unaoweza kutambuliwa kwa macho yetu. Kwa lugha ya fizikia ni sehemu ya mawimbi ya sumakuumeme yanayoweza kutambuliwa na jicho.
Mawimbi ya nuru huwa na masafa ya nanomita 380 hadi 780 au yenye marudio ya takriban terahezi 789 hadi 384.
Chanzo cha nuru duniani ni hasa jua. Nuru ya jua inaleta pia nishati inayotumiwa na mimea ambayo kwa njia ya usanisinuru inajenga kwa ndani sukari au wanga ambavyo ni lishe za viumbehai vyote vinavyozila. Hivyo nuru ya jua, kwa njia ya usanisinuru, ni chanzo cha nishati kwa karibu viumbehai vyote duniani.
Chanzo kingine cha nuru kwa binadamu ni moto. Lakini hadi karne ya 19 nuru hii ilitumia pia nishati ya jua iliyotunzwa na mimea kwa njia ya kuni, mafuta ya petroliamu au gesi asilia. Ni tangu kugunduliwa kwa umeme tu ya kwamba chanzo tofauti cha nuru kimepatikana.