Parsek (en:parsec, kifupi cha parallax second, kutoka maneno paralaksi na sekunde) ni kipimo cha umbali kinachotumiwa katika astronomia kwa kutaja umbali kati ya nyota na violwa vingine vya angani. Kifupi chake ni pc.
Umbali wa parsek 1 ni sawa na miakanuru 3.26 au karibu kilomita trilioni 31 au mita 3.0857×1016.
Ufafanuzi wa parsec ni umbali kati ya Jua na gimba la angani linaoonekana kwa pembe la paralaksi la sekunde moja ya tao (en:arcsecond).
Msingi wa kipimo hiki ni hali ya paralaksi inayosababisha ya kwamba nyota inaonekana mahali tofauti kama inaangaliwa kutoka sehemu moja kwenye obiti ya Dunia ikizunguka Jua au kutoka sehemu nyingine kinyume chake. Tofauti hii ilhali umbali wa Jua-Dunia unajulikana inaruhusu kupiga hesabu ya trigonometria na kugundua umbali wa nyota iliyopimwa.
Kwa kutaja umbali mkubwa sana kuna pia vizio vya kiloparsek (kpc), megaparsek (Mpc) na gigaparsek (Gpc).
Wanaastronomia hupendelea kutaja umbali kwa parsek kuliko miakanuru.