Semantiki (hasa huitwa: Sarufi maana) ni tawi la isimu linalojishughulisha na uchunguzi na uchambuzi wa maana za maneno, sentensi au tungo kubwa kuliko sentensi katika viwango vyote vya lugha. Hivyo ni taaluma inayochunguza na kuchambua kisayansi maana ya hisia na vitu halisi kimaneno na matumizi ya maneno kwa ujumla.
Weledi wa semantiki kwa mtumiaji ndio humsaidia mtumizi wa lugha kuitumia kwa ufaafu na kwa maadili ya mazingira husika.
Sayansi inayozungumzwa hapa ni ile ambapo lugha huchunguzwa na kuchambuliwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu maalumu zinazoihusu lugha husika. Hivyo basi kitendo cha kufuata kanuni na taratibu katika uchunguzi na uchambuzi wa lugha ni kigezo cha kisayansi.
Matawi ya isimu ni fonolojia, mofolojia, sintaksia na semantiki. Kwa mtazamo huo wa jumla wa isimu, maana ya semantiki yaweza kujengwa katika muonekano ufuatao. Semantiki ni tawi la isimu au taaluma ya isimu ambayo hufuata kanuni na taratibu maalumu katika kuchunguza na kuchambua maana ya maneno katika lugha. Maana hizo zaweza kuwa katika maneno, vifungu au sentensi, pia maana zinazoshugulikiwa ni zote, ziwe za wazi au zilizojificha.
Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Semantiki kama historia yake, uenezi au maendeleo yake? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |