Shairi (kwa Kiingereza: poem) ni aina ya fasihi. Mashairi ni tungo zenye kutumia mapigo ya silabi kwa utaratibu maalumu wa kimuziki kwa kutumia lugha ya mkato, lugha ya picha na tamathali za semi.
Mashairi ndiyo fasihi pekee duniani ambayo huingizwa katika fasihi andishi na fasihi simulizi.
Mashairi huweza kuandikwa au kutungwa kulingana na jinsi yanavyoonekana. Hii ina maana kuwa, mashairi huweza kutofautishwa kwa idadi ya mishororo, jinsi maneno yalivyopangwa, urari wa vina na kadhalika. Mtu anayetunga shairi huitwa malenga. Mtu anayekariri au kuimba shairi huitwa manju.
Kuna mashairi yanayofuata taratibu za kimapokeo, yaani yanazingatia taratibu za urari na vina, mizani, idadi sawa ya mistari, vituo na beti. Mashairi hayo huwa na mizani 14 au 16 katika kila mstari, yaani mizani 7 au 8 kwa kila kipande cha mstari.
Pia kuna mashairi yasiyofuata utaratibu huo wa kimapokeo na huitwa mashairi ya kimamboleo. Mashairi hayo mara nyingi ni nyimbo.