Unururifu (kwa Kiingereza radioactivity; pia: mbunguo nururishi kutoka Kiingereza radioactive decay) ni tabia ya elementi kadhaa ambazo kiini cha atomi yake si thabiti, bali inaweza kubadilika kuwa kiini cha atomi kingine na katika mchakato huu kinatoa mnururisho. Wakati wa badiliko atomi inatoa chembe nyuklia. Mifano ya elementi ambazo si thabiti ni urani na plutoni.
Kwa jumla elementi zote ambazo zina masi kubwa kuliko risasi (plumbi) ni nururishi. Hizi ni zote katika jedwali la elementi kuanzia namba 83 Bismuti.
Kuna pia hali za elementi kadhaa ambazo kwa kawaida ni thabiti lakini baada ya kupokea nyutroni ya nyongeza zinakuwa nururishi. Kwa mfano kaboni ya kawaida inayoitwa 12C ni thabiti. Lakini kuna pia kiwango kidogo cha 14C ambayo si thabiti, ni nururishi; hali hii huitwa isotopi cha kaboni. Kaboni ya 14C inatengenezwa mfululizo katika tabaka za juu ya angahewa ya dunia ambako atomu za nitrojeni zinagongwa na miale ya jua na kupotewa na nyutroni; hizi nyutroni zinaweza kugongana tena na atomi ya nitrojeni na kujiunganisha nayo na hivyo kuunda atomi ya 14C.
Tabia hii ya unururifu ilitambuliwa mara ya kwanza na Antoine Henri Becquerel mwaka 1896, halafu ni Marie Curie na Pierre Curie waliotunga neno "radioactivity" (=unururifu) kwa tabia hii. Wote watatu walipokea Tuzo ya Nobel ya Fizikia kwa kazi hii mwaka 1903.