Wakarismatiki ni Wakristo wa madhehebu mbalimbali ambao hasa kuanzia miaka ya 1960 wameathiriwa na tapo la Wapentekoste lililoanza Marekani mwaka 1907.
Kwa sababu hiyo wanajali karama (kwa Kigiriki χάρισμα, kharisma, yaani "zawadi", kutokana na χάρις, kharis, "neema" au "fadhili") za Roho Mtakatifu kama zilivyojitokeza katika Kanisa la mwanzo, hasa katika jumuia zilizoanzishwa na Mtume Paulo, kama ile ya Korintho (Ugiriki).
Mwaka 2011, Wapentekoste na Wakarismatiki pamoja walikuwa milioni 584, sawa na zaidi ya robo ya Wakristo wote na 8.5% ya watu wote duniani.[1]Kati yao milioni 120 ni waamini wa Kanisa Katoliki, ambalo peke yake lina Wakristo wengi kuliko tapo hilo.