Wakatoliki wa Kale ni jina linalotumika kujumlisha Wakristo wa Magharibi ambao wametengana na Askofu wa Roma hasa baada ya Mtaguso wa kwanza wa Vatikano (1869-1870) kutangaza dogma ya Papa kutoweza kukosea anapotamka rasmi jambo fulani kama fundisho la kudumu moja kwa moja.
Wakristo hao walijipatia uaskofu halisi katika mlolongo wa Mitume kupitia Askofu wa Utrecht mwaka 1873, na baada ya hapo waliusambaza kwa madhehebu mengi, ambayo mengine kwa sasa hayana ushirika nao.
Kumbe Wakatoliki wa Kale wana ushirika na Waanglikana.
Imani na liturujia zao zinafanana na zile za Kanisa Katoliki, lakini taratibu zimekwenda mbali, kwa mfano kwa kukubali upadri kwa wanawake na kwa kiasi fulani ushoga.
Baadhi ya Makanisa ya namna hiyo yanaunda "Umoja wa Utrecht" ulioanzishwa mwaka 1889 na kuwa na waamini 115,000 duniani mwaka 2016, wakiwa karibu wote wakazi wa Ulaya Magharibi na Poland.