Wakikuyu (pia: Wagikuyu) ni kabila kubwa nchini Kenya lenye watu milioni 8.1 au asilimia 17 za Wakenya wote[1]. Wenyewe hujiita Agĩkûyû. Neno Gikuyu linatokana na mti wa mkuyu (kwa Kik: mũkũyũ). Lakabu ya Wakikuyu ni Nyũmba ya Mũmbi, tafsiri yake ikiwa ni: nyumba ya Muumba.
Wao hukaa hasa katika nyanda za juu za Kenya ya Kati katika mazingira ya Nairobi hadi mlima Kenya. Mlima huu katika lugha yao huitwa "Kĩrĩma kĩrĩ Nyaga". Mlima huu wenye umaarufu kwa kuwa na kimo cha juu ni mahali ambapo wazee, walitolea kafara Mungu wao "Ngai".