Midomo ni sehemu za kinywa zinazokifunga na kukifungua. Takriban vertebrata wote wana midomo na wanyama wengine pia, hata wadudu wengi. Kwa lugha ya kila siku neno “mdomo” mara nyingi ni kisawe cha kinywa.
Midomo ni miwili, ule wa juu na ule wa chini. Mara nyingi maumbo yao ni tofauti, kama kwa binadamu. Mpaka wa mdomo wa juu unaenda chini kidogo kwenye katikati yake na unajulikana kama uta wa Kupido. Kivimbe kinene kilichopo katikati ya mdomo wa juu huitwa kinundu cha mdomo. Mfuo wa wima unaotokana na kati ya mdomo wa juu hadi kwenye ukuta wa pua huitwa filtro (philtrum).
Midomo ina daraka muhimu katika kuongea, lakini pia katika onyesho la uso. Kwa kawaida, midomo pia ina daraka muhimu katika kubusu. Kwa hivyo midomo ni nyeti sana, kwa sababu ngozi ni nyembamba sana. Hii pia husababisha damu kuonekana kupitia ngozi ya midomo, ikitoa midomo rangi nyekundu. Zeri ya midomo inaweza kutumika kwa midomo iliyokauka.
Wakati wa kucheza ala ya muziki kama tarumbeta, sauti huundwa na mvutano wa midomo.
Wanawake wengi hupaka rangi ya midomo, nyekundu hasa.