Kiarabu

"al-`arabiyya" - "Kiarabu"

Kiarabu (ar.: العَرَبِيَّة‎‎, al-ʻarabiyyah, kwa kirefu al-luġatu al-ʿarabiyya) ni lugha ya Kisemiti inayotumiwa na watu milioni 206 kama lugha ya kwanza[1] na milioni 246 wa ziada kama lugha ya pili. Ilhali kuna lahaja nyingi, Kiarabu sanifu (ar. الفصحى fuṣḥā) ni lugha rasmi ya nchi 22 za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na ya Mkutano wa Kilele wa Kiislamu na mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Mataifa. Kuna pia matumizi kama lugha ya kidini katika Uislamu.

Hivyo Kiarabu ni mojawapo ya lugha muhimu sana duniani ikisomwa kwa viwango tofauti na mamilioni ya waumini Waislamu wakielekea kujifunza na kuelewa kitabu cha Korani. Kama lugha ya kidini ina athari na taathira kubwa juu ya lugha nyingi ulimwenguni na juu ya ustaarabu na utamaduni wa watu na makabila tofautitofauti walio Waislamu.

Kiarabu kwa kawaida huandikwa kwa herufi za Kiarabu.

Ni lugha yenye utajiri mkubwa wa misamiati (maneno), ufasaha mkubwa wa misemo na udhibiti mkubwa wa sarufi na nahau.

Ni lugha iliyokusanya aina nyingi za mithali na mafumbo, na ina utamaduni mkubwa wa nyimbo, mashairi na misemo, nayo inakubaliwa na watu wengi duniani kuwa lugha yenye utamu wa matamshi na uzuri wa lafudhi.

Kwa kuwa Qurani Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad na Mashairi ya zama za Ujahili ndio yenye kudhibiti lugha hii isitetereke wala kubadilika na kupotea kama lugha nyingine nyingi, leo, baada ya miaka zaidi ya elfu, imebaki thabiti kama ilivyokuwa wakati ilipoandikwa Qurani, na mabadiliko yoyote yaliyotokea hayana uhusiano na lugha yenyewe ya Kiarabu, bali yana uhusiano na lahaja na vilugha mbalimbali zinazotumika na Waarabu wa sehemu fulani ya nchi au mji. Ama lugha rasmi ya Kiarabu basi imedhibitika kulingana na Qurani na Sunnah, ili maandishi hayo yaendelee kufahamika milele.

Leo, Kiarabu ni lugha ya sita ulimwenguni kwa wingi wa wanayoitumia kila siku katika maisha yao, baada ya Kichina, Kihindi, Kihispania, Kiingereza na Kibengali.

Umuhimu wa lugha hii unazidi kukua kila siku kwa sababu ya kutumika kwenye maeneo ya katikati ya ulimwengu baina ya mabara ya kale (Afrika, Asia na Ulaya) na mabara mapya ya ulimwengu (Amerika ya Kaskazini na Kusini).

Ramani inaonyesha nchi ambako Kiarabu ni lugha rasmi pekee (kijani) au lugha rasmi pamoja na lugha nyingine (buluu).
  1. https://www.ethnologue.com/language/arb Arabic, Standard kwenye tovuti ya ethnologue

Kiarabu

Dodaje.pl - Ogłoszenia lokalne